19 Machi 2011 - 20:30

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, Marekani ndio muungaji mkono mkubwa wa ugaidi wa kiserikali ulimwenguni. Ayatullah Ahmad Khatami amesema hayo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Ijumaa na kusisitiza kwamba, nguvu ya Marekani duniani imo katika hali ya kusambaratika.

Ayatullah Khatami ameashiria kumbukumbu ya tarehe 13 Aban inayosadifiana na siku ubalozi wa Marekani au pango la kijasusi lilipotekwa na wanachuo wa njia ya Imam Khomeini hapa nchini na kusisitiza kwamba, nguvu ya Marekani ulimwenguni hivi sasa imo katika hali ya kusambaratika. Aidha amesema, hivi sasa ulimwengu wa kibepari unakabiliwa na hali ya kusambaratika kutokana na kushindwa kukidhi matakwa ya wananchi. Khatibu wa Sala ya Ijumaa aidha ameashiria himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa madikteta na kusema kuwa, Washington haiwezi kukabiliana na wimbi la mwamko wa Kiislamu lilioibuka katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.